Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bigwa kimekuwa mwenyeji wa Kongamano la Vijana na Fursa Mkoa wa Morogoro, lililoandaliwa kwa lengo la kuwawezesha vijana wanaopata mafunzo kupitia Programu ya Uanagenzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kutambua na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, ajira na kujiajiri.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na vijana wanaopata mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bigwa, ambapo walipata nafasi ya kujifunza kuhusu umuhimu wa ujuzi, nidhamu ya kazi, ubunifu na matumizi sahihi ya maarifa wanayoyapata chuoni katika kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia maendeleo ya jamii.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, ambaye aliwakilishwa na Bw. Faraja Maduhu, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro. Akizungumza katika kongamano hilo, Bw. Maduhu aliwasisitiza vijana kutumia mafunzo wanayopata kama msingi wa kujiajiri, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Aidha, aliwataka vijana kuwa wabunifu, waadilifu na kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji vijana, ikiwemo Programu ya Uanagenzi, ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira na kukuza uchumi wa jamii.
Kwa upande wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bigwa, kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za chuo katika kuhakikisha vijana wanapata siyo tu mafunzo ya ufundi, bali pia mwongozo wa namna ya kutumia ujuzi huo katika maisha halisi kupitia ajira, kujiajiri na kutoa huduma kwa jamii.
Programu ya Uanagenzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu inalenga kuwajengea vijana uwezo wa vitendo katika fani mbalimbali, kuwaunganisha na mazingira ya kazi, pamoja na kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda na huduma.
Kongamano hilo limeendelea kuonesha nafasi muhimu ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bigwa katika kuwaandaa vijana wenye ujuzi, maarifa na mtazamo chanya wa kutumia fursa zilizopo kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.